
Zanzibar. Idara ya Uhamiaji Zanzibar imesema itaendelea kuimarisha ulinzi kwa wahamiaji katika maeneo mbalimbali ya utalii mjini Zanzibar ili watalii wawe wanatembea bila hofu yoyote.
Kamishna wa Idara ya Uhamiaji Zanzibar, Johari Masoud Sururu aliyasema hayo jana alipotembelea vituo maalumu “detached points” pamoja na fukwe za bahari maeneo ya Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alisema idara yake imejipanga vema kuhakikisha kuwa maeneo yote hasa yenye shughuli za kitalii katika mkoa huo yanakuwa salama kwa muda wote.
Alisema jambo la msingi ni kuwepo kwa ushirikiano kati ya masheha, wananchi, watendaji wengine wa Serikali na sekta binafsi pamoja na idara yake.
Alisema ushirikiano huo unaweza kuwa chachu ya kufikia malengo yaliokusudiwa.
Sururu alisema kuwa Mkoa wa Kaskazini Unguja ni kitovu cha shughuli za biashara na uwekezaji katika sekta ya utalii, hali inayosababisha kuwavuta wageni wengi kutoka mataifa mbalimbali duniani kutembelea maeneo hayo hivyo aliahidi kusimamia suala la ulinzi hasa maeno hayo.
“Kutokana na muingiliano wa wageni wanaoingia nchini humu, idara yangu itaendelea kuhakikisha kuwa wageni wote wanaoingia nchini wanaishi katika mazingira mazuri, lengo ikiwa ni kuona nchini yetu inafaidika kiuchumi zaidi,” alisema Sururu.
Aliwahakikishia masheha wa maeneo hayo kuwa Idara ya Uhamiaji itaendelea kushirikiana nao kwa vitendo hususani katika kupiga vita dhidi ya uhalifu wa aina zote ukiwemo udhalilishaji, uuzaji na usafirishaji wa dawa ya kulevya unaofanywa na baadhi ya wageni hapa Zanzibar.
Sheha wa Shehia ya Nungwi, Mohamed Khamis Haji alisema, “Nashukuru sana kwa ujio wako na hasa msimamo ulioutoa juu ya kuwachukulia hatua stahiki wageni wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu hapa Nungwi, hiki ni kilio chetu cha siku nyingi nasi tunaahidi tutaendelea kutoa ushirikiano unaostahiki kwa askari wa uhamiaji ili Shehia zetu ziendelee kupokea wageni wenye manufaa kwa jamii zetu na si vinginevyo”.
Idara ya Uhamiaji Zanzibar yajitosa kuwalinda watalii
Reviewed by EXUPER ASSOCIATION
on
December 09, 2017
Rating:
No comments: