
Serikali imekubali mapendekezo ya kamati ya uchunguzi ya kuunda chombo maalumu kitakachosimamia eneo la Loliondo ili kunusuru ikolojia ya Hifadhi ya Serengeti na kulinda mazingira.
Sambamba na kazi hizo, pia chombo hicho kimepewa kazi mahsusi ya kulinda mazalia ya wanyamapori, mapito yao na vyanzo vya maji.
“Baada ya kupitia mifumo mbalimbali, timu ya wataalamu ilipendekeza kuwa utumike mfumo utakaounda chombo maalumu kwa kuwa una masilahi mapana kwa pande zote husika,” inasema sehemu ya taarifa iliyotolewa jana na ofisi ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na kuongeza:
“..na unalenga kuleta amani na kufikia lengo la kuwa na uhifadhi endelevu katika eneo la Loliondo.” Taarifa hiyo ya Waziri Mkuu ilisema hayo baada ya kikao alichokiitisha juzi ofisini kwake mjini Dodoma ili kutoa mrejesho uliofikiwa na Serikali kuhusu utatuzi wa mgogoro wa matumizi ya Pori Tengefu la Loliondo ambao umedumu kwa takriban miaka 26. Pia, Majaliwa ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kuandaa muswada wa sheria utakaounda chombo hicho au mamlaka ya kusimamia eneo hilo.
Chombo hicho, kwa mujibu wa Waziri Mkuu kitalinda mazingira na eneo la mazalia ya wanyamapori, mapito na vyanzo vya maji kwa ajili ya ustawi wa hifadhi muhimu zenye maliasili na rasilimali za Taifa.
Akizungumza na wajumbe zaidi ya 60 waliohudhuria kikao hicho, Majaliwa alissema sheria itakayotungwa inapaswa kuhakikisha inawekewa masharti yanayozingatia masilahi ya jamii iliyopo katika eneo hilo, mila na desturi zao pamoja na uhusiano wao na matumizi ya ardhi.
Vilevile, aliiagiza wizara hiyo kuandaa waraka maalumu utakaowasilishwa serikalini kupitia Baraza la Mawaziri kuhusu umuhimu wa kutunga sheria mahsusi ya eneo hilo.
Alisema kuna ulazima wa kuwashirikisha wadau wote baada ya rasimu ya kwanza kukamilika ili waipitie.
Waziri Mkuu alisisitiza kuwa rasimu ya pili iwe imefanyiwa mapitio na kukamilika ifikapo Februari au Machi, 2018 ili mahitaji ya fedha yaingizwe kwenye mchakato wa bajeti ya Serikali ya mwaka 2018/19.
Majaliwa aliwataka mawaziri na makatibu wakuu wa wizara za kisekta zinazohusika na mgogoro wa matumizi ya ardhi ya Loliondo wafanye ziara kuitembelea ili wawe na uelewa mpana kuhusu changamoto zilizopo. Kikao hicho kilihudhuriwa na mawaziri wa Maliasili na Utalii; Tamisemi; Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; naibu mawaziri wa Kilimo; Maji; Mifugo na Uvuvi pamoja na Elimu. Pia, kilihudhuriwa na wakuu wa taasisi za Serikali, wawekezaji waliopo Loliondo, uongozi wa Mkoa wa Arusha, madiwani na wananchi kutoka Loliondo.
Desemba 2016, Waziri Mkuu alifanya ziara ya kikazi wilayani Ngorongoro ambako alipokea taarifa ya kuwapo mgogoro wa matumizi ya ardhi katika pori hilo. Januari 2017 aliunda kamati ya uchunguzi iliyokuwa na wajumbe 27 ambayo iliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.
Washiriki wa kikao hicho waliopata fursa ya kutoa maoni walipongeza uamuzi wa Serikali wa kuwashirikisha wananchi hadi ngazi ya chini katika kutafuta suluhu ya mgogoro huo.
Akichangia kwa niaba ya mashirika yasiyo ya kiserikali, mkurugenzi wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Pastoralist Women Council, Manda Neritiko alisema: “Huko nyuma tulikuwa tukipewa maagizo tu, Serikali imeamua hivi, Serikali imesema vile, lakini kwa awamu hii tumeweza kuitwa kwenye vikao na kutoa maoni yetu na hata kupewa mrejesho,” alisema.
Kwa upande wa wawekezaji, Scott Tineja Mollel kutoka kampuni ya AndBeyond Tanzania alisema wao wanataka kuhakikishiwa kuwapo kwa utalii wa siku zijazo.
Serikali yakubali kuiundia Loliondo chombo maalumu
Reviewed by EXUPER ASSOCIATION
on
December 08, 2017
Rating:
No comments: