
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam jana, kuhusu tamko la Wadau wa Habari na THRDC la kulaani tukio la kutoweka kwa mwandishi wa kujitegemea wa Mwananchi, Azory Gwanda. Katikati ni Katibu Mkuu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communication Limited (MCL), Francis Nanai. Picha na Salim Shao
Wadau wa habari wameungana na kutoa tamko la kulaani kuchukuliwa na kupelekwa kusikojulikana kwa mwandishi wa kujitegemea wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Azory Gwanda.
Gwanda alichukuliwa na watu wanne waliokuwa kwenye gari nyeupe aina ya Toyota Land Cruiser, Novemba 21 katika mji wa Kibiti mkoani Pwani alikokuwa anaishi na kufanyia kazi.
Tayari MCL na ndugu zake wameshatoa taarifa kwenye vyombo vya dola kuhusu kupotea kwa Gwanda.
Wadau walioungana kutoa tamko hilo jana ni Baraza la Habari Tanzania (MCT), Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Umoja wa Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Umoja wa Waandishi wa Kupambana na Dawa za Kulevya (OJADACT) na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari (UTPC).
Akisoma tamko hilo, Katibu Mkuu wa MCT, Kajubi Mukajanga alisema tukio hilo ni ukiukwaji wa haki za binadamu na uhuru wa habari nchini.
Alisema mara baada ya kupata taarifa za kupotea kwa mwandishi huyo, waliunda kamati ndogo ya uchunguzi na kuituma Kibiti kuthibitisha tukio hilo ili kuepuka kufanyia kazi taarifa zisizo na uhakika.
Kajubi alisema kamati hiyo ilithibitisha kuwa hadi sasa (jana) zimepita siku 20 tangu mwandishi huyo alipopotea bila kuwapo kwa jitihada za kutosha za kumtafuta kutoka kwa vyombo vya usalama.
Alisema kutokana na wimbi la utekaji na kutoweka kwa Watanzania, Serikali inapaswa kutia saini na kuridhia mkataba wa kimataifa kwa ajili ya ulinzi wa watu wote waliotekwa na kuwekwa kizuizini pamoja na mkataba wa kimataifa wa kuzuia utesaji na vitendo vingine vya kikatili vinavyopoteza utu wa binadamu.
Katika tamko hilo, Mukajanga aliwaomba viongozi wa siasa na Bunge kuona haja ya kujadili suala la utekaji na kupotea kwa Watanzania ili kuja na maazimio ya pamoja.
“Tunaviomba vyombo vya habari kuendelea kuuhabarisha umma juu ya kupotea kwa ndugu yetu Azory Gwanda, watetezi wa binadamu tuungane kupaza sauti zetu kwa pamoja juu ya hali hii ya watu kutoweka inayozidi kushika kasi nchini,” alisema.
Kajubi alisema vyombo vya ulinzi na usalama nchini vinapaswa kuhakikisha kila raia anaishi kwa uhuru na usalama na kwamba, jeshi la polisi lazima liwe tayari kuwalinda raia na mali zao.
Aliipongeza MCL kwa kufuatilia kupotea kwa mwandishi huyo na kuwataka wadau wengine wa habari kuwa na moyo huo bila kujali aina ya mkataba wa mwandishi wake.
Awali, Mratibu wa Taifa wa THRDC, Onesmo Ole Ngurumwa alisema wanasikitishwa na ongezeko la watu kupelekwa kusikojulikana huku kukiwa hakuna kinachofanyika kuzuia suala hilo kuota mizizi kwenye jamii.
Alisema taarifa zinaonyesha kuwa mwandishi huyo alikuwa mstari wa mbele katika kuandika taarifa mbalimbali za ukiukwaji wa haki, mauaji na matukio yanayotokana na hali ya Kibiti kiusalama.
Alisema Gwanda alikuwa akitumia haki yake kikatiba kutoa habari mbalimbali juu ya matukio hayo na kwamba huenda mazingira hayo yamesababisha usalama wake kuwa hatarini.
“Makundi ya watetezi, waandishi, wanasiasa na wasanii yamesharipotiwa kupotea na kutoweka. Kati yao wapo wanaookotwa wakiwa wameumizwa vibaya, wapo ambao hadi leo hawajulikani waliko na wengine kurudi wakiwa na hofu kubwa,” alisema Ole Ngurumwa.
Alisema anaamini kwamba suluhu ya matatizo yanayowakabili watetezi wa haki za binadamu itapatikana baada ya kuruhusiwa kuunda timu ya wawakilishi wachache kwenda kuonana na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP).
Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Francis Nanai aliwashukuru wadau wote vikiwamo vyombo vya habari na watetezi wa haki za binadamu kwa jitihada zao za kusaidia kumtafuta Gwanda, ambaye mpaka jana hakukuwa na taarifa za kupatikana kwake.
“Niwapongeze Watanzania wote na Rais John Magufuli kwa kusherehekea miaka 56 ya uhuru, lakini inasikitisha kuona wakati tunasherehekea Uhuru wetu leo (jana) tunaongelea suala la kuingiliwa kwa uhuru wa vyombo vya habari. Ni suala linalotia wasiwasi kidogo,” alisema Nanai.
Alisema tangu Gwanda alipopotea, hakuna fununu zozote kwamba alikamatwa na nani, kwa sababu na maelekezo yapi.
“Nizidi tu kuomba Watanzania wenye mapenzi mema, mashirika mbalimbali, vyombo vya habari, vya ulinzi na usalama vitusaidie kumpata ndugu yetu akiwa hai na mzima wa afya njema,” alisema.
Alisema mwandishi huyo anategemewa na familia yake hasa mkewe ambaye ni mjamzito.
Mashirika yaungana kulaani kupotea mwandishi wa MCL
Reviewed by EXUPER ASSOCIATION
on
December 09, 2017
Rating:
No comments: