To Advertise here call +255786419829

To Advertise here call +255786419829

Rais Magufuli aweka historia

Rais John Magufuli amevunja rekodi kwa kusamehe wafungwa 8,157 ikiwamo familia ya mwanamuziki wa dansi, Nguza Vicking ‘Babu Seya na mwanaye Johnson Nguza ‘Papii Kocha’.
Rais Magufuli alitangaza uamuzi huo jana wakati akihutubia maadhimisho ya sherehe ya miaka 56 ya Uhuru wa Tanganyika zilizofanyika mjini Dodoma na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi wakiwamo viongozi mbalimbali wa Serikali na wastaafu.
Akiwa anaelekea kumaliza hotuba yake, Rais Magufuli alisema katika kutekeleza kwa vitendo Ibara ya 45 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoeleza kuwa; “Bila kuathiri masharti mengine yaliyo katika Ibara hiyo, Rais anaweza kutenda lolote kati ya kutoa msamaha kwa mtu yeyote aliyepatikana na hatia mbele ya mahakama kwa kosa lolote na anaweza kutoa msamaha huo bila masharti au kwa masharti kwa mujibu wa sheria.
“Kipengele (b) kinasema Rais anaweza kumwachilia kabisa au kwa muda maalumu mtu yeyote aliyehukumiwa au kuadhibiwa kwa ajili ya kosa lolote na ili mtu huyo asitimize adhabu hiyo au asitimize adhabu hiyo kwa muda huo maalumu.

“(c) Kuibadilisha adhabu yoyote aliyopewa mtu yeyote kwa kosa lolote wakati kipengele cha (d) kinaeleza kufuta adhabu yote au sehemu ya adhabu aliyopewa mtu yeyote kwa ajili ya kosa lolote.”
Baada ya nukuu hizo, Rais Magufuli alisema, “Nimeona nizungumze haya ili waone nimepitia kwelikweli katika masuala ya sheria na nimepata ushauri wa kutosha,” kisha akatangaza uamuzi huo wa kusamehe wafungwa 8,157 na kuanza kubainisha walivyosamehewa.
Muda wote alipokuwa akitaja aina ya wafungwa na misamaha yao, wananchi walionekana kuwa watulivu na kufuatilia kwa makini lakini alipotaja jina la Babu Seya uwanja mzima ulilipuka kwa shangwe hali iliyomfanya kukaa kimya kidogo akisubiri utulivu.
Baada ya kunyamaza, Rais Magufuli aliendelea kusema: “Nimeamua kumsamehe Nguza Vicking, jina lingine anaitwa Babu Seya na ndugu Johnson Nguza au Papii Nguza (Kocha) nao waachiwe huru kuanzia leo (jana),” alisema Rais Magufuli huku wananchi wakiendelea kushangilia kwa nguvu.
Akizungumzia msamaha wa wafungwa 8,157 Rais Magufuli alisema kati yao 1,828 walitarajiwa kuwa huru jana na waliobaki 6,329 wamepunguziwa muda wa kukaa gerezani na watatoka gerezani kulingana na vifungo vyao.
Pia Rais aliwasamehe wafungwa 61 waliohukumiwa kunyongwa ambao hawakutenda makosa ya kuua walemavu wa ngozi au ujambazi.
“Watu hawa wafanyiwe mchakato wa kutolewa leo (jana) au kesho (leo), kulingana na taratibu zinavyokwenda. Nimefanya hivi kwa hali halisi niliyoiona kwa hawa watu, yupo mtu aliyefungwa akiwa na miaka 18 na sasa ana miaka 60 na kitu,” alisema Rais Magufuli.
Alieleza kuwa kati ya watu hao yumo Mzee Mtanga Matonya mwenye umri wa miaka 85 ambaye ameshakaa gerezani kwa miaka 37 mbali na miaka saba aliyokuwa mahabusu akisubiri hukumu yake, hivyo ukimjumilisha ni jumla miaka 44.
Alisema orodha hiyo aliyoitoa atamkabidhi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ili ashughulikie mapema kupitia kwa vyombo husika.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu atahakikisha hawa watu wasiongezewe majina mengine au majina kupunguzwa na mimi nasaini hiki kielelezo mbele ya wananchi wa Dodoma, watani zangu ili watu hawa kesho wawe wametoka,” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli alisema wafungwa waliohukumiwa kunyogwa katika Gereza la Uyui (Tabora) wapo wawili, Butimba (Mwanza) watano, Ruanda (Mbeya) wanne, Isanga (Dodoma) 15, Maweni (Tanga) 11, Kingolwira (Morogoro) watano na Ukonga (Dar es Salaam) 19.
“Kwa vyovyote watani zangu Wazaramo humu wataponapona,” alisema Rais Magufuli na kuibua kicheko kwa watu waliohudhuria alipokuwa akizungumzia wafungwa 19 wa Ukonga waliosamehewa.
Alisema hadi juzi, Tanzania ilikuwa na wafungwa 39,000, kati yao wanaume 37,000 na wanawake 2,000.
“Wafungwa waliohukumiwa kunyongwa hadi juzi ni 522 kati yao wanaume ni 503 na wanawake 19, hivyo wanaosubiri kunyongwa wengi ni wanaume.
“Wafungwa waliohukumiwa maisha ni 666 kati yao wanaume ni 6,55 na wanawake 11, kwa hiyo magereza ya Tanzania wengi waliofungwa maisha na wanaosubiri kunyongwa ni wanaume. Tuanze kujitambua sisi wanaume kwa nini tupo hivi,” alisema JPM.
Rais Magufuli aweka historia Rais Magufuli aweka historia Reviewed by EXUPER ASSOCIATION on December 09, 2017 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.