
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan
Arusha. Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewataka wataalamu wa ununuzi na ugavi kuzingatia utaratibu na sheria zinazosimamia taaluma ili kuendana na kauli mbiu ya Serikali ya kubana matumizi yasiyo ya lazima.
Akizungumza leo Jumatatu Desemba 4,2017 kwenye kongamano la nane la Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) jijini Arusha, ametaka litumike kuelezana ukweli, kukemea bila woga wala vitisho vitendo vinavyotia doa taaluma hiyo.
"Mnapaswa kuwawajibisha wote wanaochafua kada hii kwa kutekeleza majukumu yao kinyume cha utaratibu na sheria; ni dhahiri watu hawa ni kansa na hawafai kuwa miongoni mwenu," amesema.
Akizungumzia kauli mbiu ya kongamano hilo, “Mchango wa wanataaluma wa ununuzi na ugavi katika kukuza uchumi wa viwanda” amesema inaendana na dhamira ya Serikali inayotaka kukuza sekta ya viwanda na miundombinu wezeshi.
Samia ameitaka Wizara ya Fedha na Mipango kukamilisha haraka sera ya Taifa ya ununuzi na ugavi wa umma kwa kuwa ndiyo mwongozo na msingi wa kufanya marekebisho ya sheria, kanuni na utaratibu utakaoongoza shughuli za ununuzi wa umma nchini.
Pia, amewataka waajiri katika idara na taasisi za umma kuajiri wataalamu wa ununuzi na ugavi waliosajiliwa na PSPTB ili kutekeleza matakwa ya kisheria.
Awali, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema lengo la bodi ni kuliwezesha Taifa kupata thamani halisi ya huduma na bidhaa inayolingana na kiasi cha fedha kilichotumika kuzinunua.
Samia atoa angalizo kwa wataalamu wa ununuzi, ugavi
Reviewed by EXUPER ASSOCIATION
on
December 04, 2017
Rating:
No comments: